Nyota ya Mashariki
Nyota ya Mashariki Lyrics
- Kakukirimia, uwe ulivyo,
Atakutumia impendezavyo
Akikuinua, inuka, hivyo,
Ninakuombea heri vilivyo;
Hakunipa hayo, nikuhitaji,
Kwa niliyo nayo, upate maji,
Na mwisho wa hayo, tuvikwe taji,
Tuingie nayo, wa mbingu mji.
{ Nimeiona nyota yako mashariki (nyota yako)
Ninajivuna inavyong'ara rafiki (helelelele)
Naandamana kuja unakotamalaki
Kumsujudia Bwana aliyekupa milki (ho ndugu) } *2
- Sirudi kwa njia, yake herode,
Anakuvizia, kila upande,
Wivu unamjia, kakunja, konde,
La kukuzuia juu usipande;
Ni kama Kaini, mwua Abeli,
Au Raubeni, wa Israeli,
Waliotamani, kuzika, hali,
Ya wadogo duni, wake Jalali!
- Ninakuombea, usife moyo,
Maana dunia, si rafikiyo,
Wewe fuatia, za Kristu, nyayo,
Aliyekufia, kwa mizigoyo;
Wa ulimwenguni, watakufumba,
Wazuri machoni, moyo mwembamba,
Hawatatamani, uitwe, mwamba,
Ni wivu moyoni, unawasomba!