Tunakutukuza
Tunakutukuza Lyrics
- Pande zote za dunia, viumbe wako wote wakushangilia,
Watu wanakuinua, nasi tunakuimbia;
Umekuwa mwaminifu, watukumbuka sisi tulio dhaifu,
Tusojua kukusifu, wewe mwenye utukufu.
Kwa zeze na vinanda - tunakutukuza
Baragumu na panda - tunakutukuza
Nderemo zimetanda - tunakutukuza
Na ngoma zinadunda - tunakutukuza
Iyee (ae hoye) , aiyee (ae hoye ) aiyee (ae hoye) tunakutukuza
Aiyee (ae hoye) , aiyee (ae hoye ) aiyee (ae hoye) tunakutukuza
- Sina budi kushukuru, ulinivua giza kanivika nuru,
Utumwa kaninusuru, kaniweka niwe huru;
Japo mimi hukosea, hujanitupa bado wanihurumia,
Hata ninapopotea, wanielekeza njia.
Kwa nyimbo na zaburi - tunakutukuza
Filimbi na zumari - tunakutukuza
Kayamba na matari - tunakutukuza
Na kwa sauti nzuri - tunakutukuza
- Unipaye bure hewa, kunitetea kila ninapoonewa,
Kwako sijapungukiwa, wala sijaelemewa;
Unayenipa mkate, na kunilinda kote wakati wowote,
Nijalie nisisite, kukusifu siku zote.
Sifa zote ni zako - tunakutukuza
Huko juu uliko - tunakutukuza
Vigelegele, heko - tunakutukuza
Na shangwe na chereko - tunakutukuza
* * *
Una neema tele - tunakutukuza
Tangu enzi za kale - tunakutukuza
Na umebaki vile - tunakutukuza
Milele na milele - tunakutukuza
Wasio na chakula - unawapokea
Wasona pa kulala - unawapokea
Wajapo kwako bila - unawapokea
Unawajibu sala - unawapokea
* * *
Vipofu wanaona - wanakutukuza
Viwete wanapona - wanakutukuza
Tasa wapata mwana - wanakutukuza
Na bubu wananena - wanakutukuza
Kweli wewe ni baba - tunakutukuza
Daima watubeba - tunakutukuza
Kwako twapata tiba - tunakutukuza
Watukinga misiba - tunakutukuza